Thursday 8 January 2015

Yanga yamtema rasmi Kaseja

Mkuu wa Idara ya habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro akiongea na waandishi wa habari leo
Na Bertha Lumala
Uongozi wa mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara, Yanga SC umetangaza rasmi kumtema kipa mzoefu Juma Kaseja baada ya kuvunjwa kwa mkataba wake.
Ikumbukwe kuwa Desemba 31, mwaja jana, Yanga SC iliwasilisha orodha ya wachezaji 24 katika Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kwa ajili ya michuano ya mwaka huu ya Kombe la Shirikisho, ikiwa na makipa watatu; Deogratius Munishi ‘Dida’, Ali Mustafa ‘Barthez’ na Alphonce Majogo huku jina la Kaseja likikosekana katika orodha hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Zanzibar Ocean View mjini Unguja leo mchana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro amesema klabu hiyo imeamua kuachana na kipa huyo chaguo la kwanza la zamani la Taifa Stars kutokana na kukiukwa kwa masharti ya mkataba kati ya pande hizo mbili.
Muro amesema kuwa Novemba 8, 2013, usajili wa miaka miwili wa Kaseja Yanga ulifanyika akipewa Sh. milioni 20 za utangulizi kati ya Sh. milioni 40 za ada ya kusaini mkataba kuitumikia klabu hiyo ya Jangwani.
Ameendelea kufafanua kuwa Januari Mosi, 2014 Yanga ilimlipa Kaseja Sh. milioni 20 alizokuwa akiidai ikiwa ni ada ya usajili.
Hata hivyo, Muro amesema Kaseja aliwasilisha barua Yanga Novemba 11, 2014 akilalamika kutopangwa mara nyingi kwenye kikosi hicho cha wanajangwani huku pia akitaka kukatiwa bima.
“Desemba 12, 2014 Yanga ilimjibu Kaseja kwamba taratibu zote anazijua kuhusu masuala ya bima za matatizo makubwa ya wachezaji ‘serious injuries’ na kumkumbusha kuwa suala la kupangwa kikosini liko chini ya benchi la ufundi.
“Isitoshe Kaseja alipangwa katika mechi nyingi za Yanga, alicheza dhidi ya Mtibwa Sugar, CDA ya Dodoma na timu moja ya Shinyanga. Katika michezo tunajua mchezaji hawezi kuwa ‘fiti’ wakati wote.
“Desemba 31, 2014 akaleta barua nyingine akidai suala la bima na kutopangwa katika mechi nyingi. Tukaona Juma Kaseja hana hoja za msingi, kama imeshalipwa, kwa nini aendelee kuwa hivyo? Tukaona hapa kuna kitu.
“Msimamo wa klabu tunamwacha aende zake. Usipoonekana katika kambi na mazoezi ya timu yetu kwa siku mbili bila kutoa taarifa, kwa mujibu wa mikataba ya Yanga na wachezaji, unakuwa umevunja mkataba.
“Kama yeye alimwaga mboga, na sisi (Yanga) tunamwaga ugali,” amesema zaidi Muro aliyekuwa amefuatana na kocha mkuu Mholanzi Hans van der Pluijm na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

No comments:

Post a Comment

TEAM PARTICIPATING